Ligi ya mabingwa ulaya iliyoendelea
jana usiku, tulishuhudia mechi za makundi manne tofauti. Kwa upande wa kundi D
tulishuhudia mechi mbili, mojawapo ikiwa kati ya Arsenal na Galatasaray.
Arsenal ikiwa katika uwanja wake wa nyumbani wa Fly Emirates iliweza kuibuka na
ushindi mnono wa bao 4 kwa 1 dhidi ya mabingwa
wa Uturuki. Mchezo huo ulioanza kwa kasi sana huku ukiwa na mashambulizi
ya kupokezana na kushtukizana kulingana na aina ya mchezo wa timu hizo mbili,
Galatassaray kupitia kiungo wake maridadi kabisa Wesley Sneijder iliweza
kushambulia katika lango la Arsenal ndani ya dakika 15 za mwanzo. Lakini
baadaye hali ilibadilika baada ya Danny Welbeck kuiandikia Arsenal goli la
kwanza na pia goli la kwanza la Welbeck katika ligi ya mabingwa ulaya katika
dakika ya 22, goli hilo lilionesha kuanza kujiamini kwa mshambuliaji huyo
liliwekwa wavuni baada ya Welbeck kupokea pasi ya shukrani kutoka kwa Alexis
Sanchez. Dakika nane baadaye Welbeck aliutumia uzembe wa mabeki wawili wa
Galatasaray na kujitangulizia mpira kwa kichwa mpaka kwenda kutikisa nyavu za
Galatasaray na kuiandikia timu ya Arsenal goli la pili. Alexis Sanchez
aliyeonekan kuisumbua sana safu ya mabeki wa Galatasaray kwa kumiliki mpira na
kuukokota kama ilivyo kawaida ya mchile huyo, Lakini Felipe Melo alimfanyia
madhambi mchile huyo dakika ya 34 na kupata kadi ya njano kutoka kwa muamuzi.
Hata hivyo madhambi yale hayakutosha kupunguza kasi maana dakika 7 baada ya
kufanyiwa madhambi Sanchez alizamisha goli la tatu baada ya kuitendea haki pasi
ya kiungo mjerumani Mesuit Ozil kwa kuwafinya mabeki na kutia wavuni mpira
uliompita kipa Fernando Muslera. Kipindi cha kwanza kilimalizika Arsenal ikiwa
mbele kwa mabao 3 kwa 0.
Kipindi cha pili kilianza kwa mabadiliko
kutoka kwa kocha Cesare Prandeli baada ya kumtoa Yekta Kurtulus na kumuingiza
kiungo mwenye uzoefu mkubwa aliyewahi kuichezea Real Madrid, Hamit Altintop.
Kipindi cha pili kilichoanza kwa kasi zaidi hasa kwa hawa washika bunduki wa
London ambao dakika ya 52 kupitia kwa mshambuliaji wao mpya Danny Welbeck
aliyewatoka mabeki wa Galatassaray na kwenda kumalizia pasi maridadi kutoka kwa
Alex Chamberlain na hivyo kujiwekea “hat trick” yake ya kwanza katika maisha yake
ya soka.Na hivyo kuifanya sherehe ya kutimiza miaka 18 ya Arsene Wemger ya
kuifundisha klabu ya Arsenal kuwa nzuri zaidi. Uzembe mkubwa uliosababishwa na
mabeki wawili wa kati wa Arsenal ulimfanya golikipa Szczesny kufanya uamuzi
mgumu na kuamua kumfanyia madhambi Mshambuliaji wa Galatassaray Burak Yilmaz
katika eneo hatari na kuambulia kadi nyekundu pamoja na “penati” dhidi ya
Arsenal. Dakika hiyo ya 62 ilimlazimu Arsene Wenger kufanya mabadiliko na
kumuingiza golikipa Ospina na kumtoa Alexis Sanchez ili kunusuru ushindi wake.
Hata hivyo David Ospina hakutosha kuzuia mpira wa penati uliopigwa kwa ufundi
mkubwa na kuipa Glatassaray goli la kufutia machozi lilodumu mpaka mwisho wa
mechi. Mabadiliko yalifanyika katika timu hizi mbili, kwa upande wa Arsenal iliyomtoa
Oxlade Chamberlain na Mesut Ozil na kuwaingiza ili Tomas Rosicky na Jack
Wilshere walio wakabaji zaidi ili kupoza
mashambulizi. Kwa upande wa Galatassaray Bruma na Umut Bulut waliingia
kushika nafasi ya mkongwe Pandev na Veysel Sali ili kuongeza nguvu ya
ushambuliaji na kutumia nafasi ya wachezaji kumi wa Arsenal. Hata hivyo kicwa
kilichopigwa na mshambuliaji Burak Yilmaz kiliweza kuokolewa na golikipa Ospina
na baadaye Santi Cazorla alitumia pasi ya Jack Wilshere vizuri, lakini mabeki
wa Galatassaray waliuzia mpira ule karibia na mstari. Matokeo yalimalizika
Arsenal ikiwa kifua mbele kwa goli nne (4) kwa moja(1) dhidi ya Galatasaray na Welbeck
kuonekana kuwa nyota wa mchezo huo.
Matokeo
mengine ni Borrusia Dortmund aliweza kuibuka na ushindi wa mabao matatu kwa
bila dhidi ya Anderlecht, Atketico Madrid iliyopata ushindi wa bao 1 kwa 0
dhidi ya Juventus bao liliofugwa na Arda Turan, Malmo ilijipatia ushindi wa
mabao 2 kwa 0 dhidi ya Olympiakos, Majogoo wa wingereza Liverpool Fc waliambulia
kichapo cha bao 1 kwa 0 kutoka kwa wababe Fc Basel, Real Madrid wakiwa ugenini
walipata ushindi wa mabao 2 kwa 1 dhidi ya wenteji wao Ludogoret, Byer
Leverkusen ikiwa katika uwanja wake wa nyumbani iliweza kuibuka na ushindi
mnono wa mabao 3 kwa 1dhidi ya Benefica nao Zenit na Monaco walitoka suluhu ya
bila kufungana katika uwanja wa nyumbani wa Zenit.
Na,
Kelvin Kiimbila Jr,
0719580495,