Wiki tatu
zilizopita moja wa magwiji wa soka Duniani Johan Cryuff alimualika Xavi
Hernandez kufungua moja ya kiwanja cha soka kwa ajili ya vijana wa
mtaanii.Kiwanja hiko kilichofunguliwa kwenye mtaa wa Terrassa nchini Spain
kilipewa jina la Xavi.Xavi ambaye mitandao mingi Duniani inamtambua kama
mchezaji bora wa muda wote katika nchi ya spain alikuzwa katika viwanja hivyo
vya mtaani kabla hajachukuliwa na klabu ya Barcelona akiwa na umri wa miaka
11.Kwenye karne yetu hakuna mchezaji
fundi wa kupiga pasi kuliko Xavi.Umaridadi wote wa Xavi tumeuona
kwasababu ya viwanja bora alivyocheza tangu
akiwa chipukizi mpaka hivi sasa.Usingeweza kuuona na wala huwezi kuuona
kamwe Ubora na pasi maridadi za Xavi kama siku moja atacheza kwenye uwanja kama
wa jamhuri.Bado nawaza kama Xavi angezaliwa
Tanzania?.Bila shaka tusingeweza kuona utamu wa miguu ya xavi hasilani kama
tunavyoona akiwa kwenye uwanja wa camp nou.
Wakati
naangalia mechi ya Simba na Mtibwa nikamuwaza Xavi Hernandez,Nikafikiria kama
angeweza kufanya kile alichoshindwa kufanya mkude ndani ya uwanja wa
jamhuri.Nikagundua ningemuonea huruma Xavi kama nilivokua nauonea huruma mguu wa mkude.Kila
akijaribu kuonesha thamani ya mguu wake nyasi za uwanja wa jamhuri ziligeuka
kuwa kizingiti kwake.Pasi ya mkude kabla ya kumfikia Ndemla lazima ipite kwenye
mashimo matatu ya uwanja wa jamhuri.Kabla ya kumfikiria Shaban Nditi kuzuia
mpira lazima kwanza ufikirie ni jinsi gani ya kukwepa mashimo hayo
yaliyokithiri kwenye uwanja wa Jamhuri.Ubovu wa uwanja wa jamhuri haukuwa na
athari kwa simba pekee bali hata kwa wenyeji Mtibwa Sugar.Si Simba wala Mtibwa
iliyopiga pasi nyingi kuliko mashimo ya uwanja wa jamhuri.Kama ningekuwa natoa
takwimu za umiliki wa mpira ningetoa 40% kwa mashimo na nyasi za uwanja wa
jamhuri,32% kwa Simba na 28% kwa Mtibwa Sugar.
Uwanja wa
jamhuri si kiwanja kibovu pekee Tanzania bali ni mfano wa kiwanja kibovu
Tanzania.Ukiondoa Uwanja wa Taifa na Chamanzi hakuna kiwanja kingine
kinachotumiwa kwenye ligi kuu Tanzania chenye sehemu nzuri ya kuchezea mpira.Ntaanzaje
kumhukumu coutinho au Niyonzima kama
anacheza kwenye uwanja mbovu kama wa kaitaba.Ntapataje ujasiri wa kuanza kuiita
ligi yetu bora kama viwanja tulivyonavyo ni vile vile vya enzi za mwalimu.?
Kwa hili
ntailaumu Tff pamoja na wamiliki wa
viwanja hivyo. Tanzania ni sehemu pekee ambapo viwanja vya mpira wa miguu
haviheshimiwi.Sijawai kusikia hata siku moja msanii kutoka uingereza anafanyia tamasha lake la muziki kwenye uwanja wa
wembley au Old Traford.Lakini Tanzania uwanja huo huo wa kuchezea mpira pia
kufanyia matamasha ya muziki.Tena mara nyingine utakuta leo kuna tamasha la
muziki na kesho kuna mechi ya Mtibwa na Simba kwenye uwanja huo huo
mmoja.Matamasha hayo yanachangia kwa kiasi kikubwa uharibifu wa viwanja vya
soka, Hakika vitendo hivo ni kuukosea heshima mchezo wa soka.
Kwa upande
mwingine timu zinapocheza kunakuwa na mapato kwa ajili ya viwanja.Lakini mapato
hayo huwa hayendi kwa ajili ya matengenezo ya viwanja husika zaidi ya kuishia
kwenye matumbo ya wahusuda wachache.Wamiliki wa viwanja wanajali kujinufaisha
tu na viwanja hivyo pasi na kujali ubora wa viwanja vinavyowaingizia mapato.
Nikirudi
kwa upande wa Tff ntawalaumu kwa kushindwa kuweka masharti ya vigezo vya
viwango vya viwanja vinavyopaswa kutumiwa kwenye ligi kuu Tanzania.Tff ingekuwa
na msimamo mkali kwa wamiliki wa viwanja tusingekuwa na viwanja vibovu Tanzania.Tatizo
la shirikisho letu wamekubali kuwa bidhaa rahisi kwa kila kitu kinachohusu
makubaliano.Viwanja vya Tanzania kwa asilimia kubwa vinamilikiwa na chama cha mapinduzi.Kila siku huwa
najiuliza kwanini chama hiko hakitaki kuachia viwanja hivyo kwenye mamlaka za
soka ilihali wameshindwa kuvikarabati na
kuvisimamia viwanja hivyo.Nchi kama spain ilijenga viwanja vya soka ila ilipo
ona majukumu yamezidi wakaamisha umiliki wa viwanja kwa timu husika za ligi
kuu.
Kama CCM
haitakubali kurekebisha Viwanja hivyo
sambamba na kutoruhusu mambo mengine yasiyohusu soka kufanyika ndani ya viwanja
vya soka,Pia kama hawatakubali
kubinafsisha viwanja kwa mamalaka za soka basi tutaendelea kushuhudia viwanja
vyetu kupiga pasi nyingi kuliko mkali Xavi Hernandez.
Na
Allen Kaijage
0655106767
kaijagejr@gmail.com