Mzunguko wa tano wa Ligi Kuu ya Wanawake hatua ya nane bora unatarajia kuendelea Jumapili Aprili 21, mwaka huu kwenye viwanja tofauti.
Ligi hiyo ilisimama kwa muda kupisha maandalizi ya Timu ya Taifa ya Wanawake (Twiga Stars) iliyokuwa kambini kujiandaa na mchezo wake wa kufuzu fainali za Afrika kwa wanawake.
Hatua hiyo ya nane bora inachezwa kwa mtindo wa nyumbani na ugenini ikishirikisha Timu za Panama FC ya Iringa inayotumia Uwanja wa Samora, Evergreen Queens ya Dar es Salaam inayotumia Uwanja wa Karume na JKT Queens ya Dar es Salaam wanaotumia Uwanja wa Mbweni,
Timu nyingine ni Alliance ya Mwanza wanaotumia Uwanja wa Nyamagana, Mabingwa watetezi Mlandizi Queens ya Pwani wanaotumia Uwanja wa Mabatini, Baobab ya Dodoma wanaotumia Uwanja wa Jamhuri Dodoma, Kigoma Sisters ya Kigoma wanaotumia Uwanja wa Lake Tanganyika na Simba Queens wanaotumia Uwanja wa Karume.
Huu ni msimu wa pili kwa Ligi ya Wanawake kuchezwa ambapo katika msimu wake wa kwanza Timu ya Mlandizi Queens ndiyo waliibuka na ubingwa.