Pichani Lwandamina akishuhudia mchezo wa Zesco Zambia
MAMBO bado mazito na mashabiki wa Yanga hawaelewi nini kimetokea hadi kocha, George Lwandamina akaondoka kwenye kikosi cha mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu Bara.
Mabosi nao wamepigwa na mshangao na kulazimika kukutana kwa dharura kujadili suala hilo kwa kina, lakini Lwandamina mwenyewe jana amefunguka huku akieleza sababu sita zilizomuondoa klabuni hapo.
Mbali na kufichua sababu hizo, pia ametoa masharti mazito kwa uongozi wa Yanga akitaka kung’olewa kigogo mmoja, ambaye amedai amekuwa kikwazo katika utendaji kazi wake.
Akizungumza na Mwanaspoti katika mahojiano maalumu yaliyodumu kwa saa 1:20 jana asubuhi, moja kwa moja kutoka Ndola, Zambia, Lwandamina alisema kwa muda wote aliokuwa klabuni hapo, amekuwa akifanya kazi kwenye mazingira magumu.
Alisema kuwa mashabiki na wapenzi wa Yanga wanapaswa kufahamu kuwa, chini ya uongozi wa Katibu Mkuu wa klabu hiyo, Charles Mkwasa, amekuwa kwenye wakati mgumu kutekeleza majukumu yake.
Bila kung’ata maneno, Lwandamina amemtaja Mkwasa kuwa ndiye aliyemfanya kuchukua uamuzi mgumu wa kuiacha timu hiyo na kurejea kwao, ambako amekuwa akihusishwa kutua klabu yake ya zamani ya Zesco. Pia, straika wa kimataifa wa Zimbabwe, Donald Ngoma naye ametajwa kwenye sakata hilo la Lwandamina.
Hata hivyo, Mzambia huyo alisema wakati Mkwasa akiteuliwa kushika wadhifa huo alipata mzuka na ujio wake akiamini atakuwa na msaada mkubwa kwake, lakini baadaye mambo yamekuwa tofauti huku akishindwa kupata ushirikiano aliotarajia.
Yanga jana ilikuwa uwanjani kuivaa Singida United na kutoka sare ya 1-1 bila uwepo wa Lwandamina kwenye benchi la ufundi na hizi ndio sababu sita za kuitosa Yanga.
*KANUNI NA TARATIBU*
```“Unajua kwanini nimeondoka Yanga, ieleweke kuwa wakati tunakaribia kufanya usajili kuna mambo tulikubaliana yafanyike na uongozi ikiwemo suala la kubadilisha mikataba ya wachezaji wetu ili kuwepo na uwajibikaji,” alisema Lwandamina na kuendelea.
“Tulikubaliana tubadilishe kanuni na taratibu za wachezaji, hizi zinazotumika sasa zimepitwa na wakati, baadhi ya wachezaji hawakuwa na uwajibikaji mzuri. Klabu inapoteza fedha nyingi, lakini inakosa huduma bora kutoka kwa wachezaji ili kuiwezesha timu kusonga mbele. Tangu wakati huo hakuna kilichofanyika.```
```“Nilimuuliza akaniambia hakupata taarifa yangu hivyo, nikamtumia tena akapokea lakini bado akashindwa kuzitafsiri na kuzifanyia utekelezaji wake, sasa hilo ni tatizo kubwa kwangu kama ninayetambua majukumu yangu.”```
*MFUMO WA MALIPO*
```“Uongozi unafahamu kuwa nimefikisha miezi mitatu sasa bila kulipwa mishahara yangu na mara ya mwisho kulipwa ilikuwa Desemba, mwaka jana. Lakini, siko Yanga kwa ajili ya kutafuta fedha na niliwahi kumshauri awe anatangulia kwanza kuwalipa wachezaji na mimi niwe wa mwisho kwa kuwa wao ndiyo watu wanaofanya kazi na waliobeba furaha za Wanayanga.```
```“Tatizo linakuja sio mtu mkweli anapokuwa amepata fedha na hataki tukae chini kutengeneza mtiririko mzuri wa malipo badala yake amekuwa akija kwenye timu na kuahidi malipo, lakini baadaye hafanyi hicho kitu.```
```“Mfano mzuri ni hivi karibuni wakati tunacheza na Township Rollers aliahidi kumaliza malipo yote ya wachezaji, lakini baada ya hapo wachezaji wakakuta wameingiziwa mshahara wa mwezi mmoja pekee na kilichotokea kila mtu aliona. Mwisho wa siku mimi ndiye nalaumiwa kwa matokeo mabaya ya timu,” alidai Lwandamina.```
*MAWASILIANO HAFIFU*
```“Wanasheria wangu wamekuwa wakiwasiliana naye kila wakati kwa njia ya barua pepe (email), lakini huwa hana kawaida ya kuwajibu. Viongozi wa kamati ya mashindano ya Yanga ndiyo walionifanya nibaki hapo, walikutana na mimi tukakubaliana niongeze mkataba kuendelea kuwepo Yanga, lakini mpaka sasa mambo yapo kimya tu.```
*MAELEWANO MABOVU*
```“Nimeishi katika mazingira magumu na Charles (Mkwasa), Yanga ina changamoto nyingi lakini bado tumekuwa tukipambana kuhakikisha timu inashinda na sasa tunakaribia kuingia hatua ya makundi na hata kwenye ligi bado tuna nafasi nzuri. Tunawafukuza kwa kasi Simba pale kileleni, lakini muulizeni kama kuna siku timu imeshinda akatuma ujumbe kupongeza au hata kupiga simu.```
```“Matokeo yetu mazuri zaidi katika mashindano ya Afrika ni hivi karibuni wakati tunawafunga nyumbani Welaytta Dicha, mtendaji huyo alikuwepo uwanjani na alishindwa hata kuja kuwapongeza wachezaji akaondoka, lakini timu ikipoteza huwa ni mwepesi kuja kutupa pole. Hapa kuna tatizo ndani yake.```
```“Niliwahi kusikia anataka kazi yangu na wala hafurahii ninachofanya Yanga, pengine anataka kazi yangu nafikiri sasa nafasi anayo. Hata huyu Mhilu, ambaye nimepambana kumtengeneza na sasa yuko vizuri aliwahi kuniambia anataka kumtoa kwa mkopo, lakini wachezaji ambao nilitaka watolewe kwa mkopo wote bado wapo klabuni mpaka sasa.```
*KUMUONA KOCHA,WACHEZAJI KAMBINI*
```“Kuna wakati kulifanyika mambo ambayo hayakunifurahisha kabisa, yalinisumbua sana. Wakati tunajiandaa na msimu mpya wa ligi mtendaji huyu aliwahi kuja kambini pale Morogoro na alipofika alikaa mbali akiangalia mazoezi. Lakini, mazoezi yalipokwisha nilitaraji kama bosi wa klabu angekuja kutusalimia na kuzungumza na wachezaji, lakini hakufanya hivyo aliondoka zake.```
```Kuna wakati tunaweka kambi hapo hoteli ya Kariakoo ni umbali mfupi sana kutoka makao makuu ya klabu, bado hakuwa anakuja kukutana na sisi kuangalia timu yake inaishi katika mazingira gani```
*MATATIZO YA NGOMA*
```“Kuna huyu mchezaji Donald (Ngoma) sijajua mpaka sasa anafanya nini klabuni na amekuwa na mfululizo wa matatizo mara anaumwa, mara amepona na akija anakataa kucheza. Tatizo limekuwa kubwa hata wachezaji muhimu zaidi wanaovuja jasho kuipigania timu sasa wanataka kuondoka. Unajua Kelvin (Yondani) na wenzake wanaweza kuondoka na sababu wanaona Ngoma kama anadekezwa na kupendelewa.```
```“Yanga ina mashabiki wakali na wenye hasira sana na ninapata shaka wasije wakaondoka wachezaji muhimu kisha nikafanyiwa vurugu. Nimeona niondoke mapema, naamini wachezaji hawa wana moyo wa kubaki Yanga na kushinda mataji. Niliwahi kushauri mambo kadhaa kuhusiana na Ngoma, lakini hakuna utekelezaji mpaka sasa na hili lina athari.```
```“Nimecheza mpira na hata amecheza katika mazingira kama haya ya wachezaji wachache kujiona ni umuhimu zaidi na kushindwa kuonyesha kazi uwanjani ni rahisi kuigawa timu.”```
*ASISITIZA BADO HAJASAINI*
```Hata hivyo, wakati mashabiki wa Yanga wakigubikwa na simanzi kutokana na kuondoka kwa kocha huyo, lakini mwenyewe amesisitiza kuwa hajasaini mkataba kuinoa Zesco.```
```Amesema yeye bado ni mwajiriwa wa Yanga kwa kuwa hajamaliza mkataba wake japo una changamoto nyingi.```
```“Sijasaini Zesco mpaka sasa ingawa presha ni kubwa ya kutakiwa kufanya hivyo, yapo mawasiliano nimefanya na baadhi ya viongozi wa Yanga na wameniomba nitulie kwanza ili wapate fursa ya kukutana.```
```Nimeona taarifa ya Zesco wameniteua kuwa kocha wao, ila sio kweli na mkitaka kudhibitisha hilo nendani kawaulize viongozi wa Yanga, mimi si mtu wa kufanya uamuzi wa haraka,” alimaliza Lwandamina.```
```Mwanaspoti lilimtafuta Mkwasa, ambaye tuhuma nyingi za Lwandamina zimeelekezwa kwake, ambapo alisema hawezi kuzungumzia tuhuma hizo kwa sasa. Alisema uongozi wa Yanga ulitarajiwa kukutana jana usiku kujadili suala la Lwandamina na baada ya hapo ndipo anaweza kuzungumza tuhuma hizo.```
```Meneja wa Yanga, Hafidh Saleh alisema kwa sasa timu itakuwa chini ya Nsajingwa, ambaye yupo vizuri na anaweza kuiongoza ikapata matokeo.```