Breaking News
Loading...
Saturday, 2 August 2014

Info Post



Ni alhamis ya leo ambayo Dunia macho na msikio yake yanaelekezwa nchini Brazil ,katika michuano mikubwa kabisa maarufu kama kombe la Dunia safari hii ikishirikisha mataifa 32 na Afrika tukiwakilishwa na Mataifa matano ambayo ni Nigeria,Cameroon,Ivory Coast,Ghana na Algeria,basi tunawaombea kila ra heri wawakilishi wetu angalau mwaka huu na si tujitoe kimasomaso,basi turudi nyumbani tujulishane mambo yetu.

Kwa wale Binadamu waliokuwa na kulelewa  au kupita katika Mkoa wa Tabora  mji mashuhuri kwa jina la mashujaa wa Unyanyembe watanielewa vizuri,Mkoa huo ni maarufu mno kwa zao la Embe kuna maembe ya aina nyingi tu Mkoani pale lakini nayatazama ya aina mbili tu,kuna Embe Dodo na Embe Bolibo,desturi na kawaida ya embe dodo ni chungu mno likiwa bichi lakini ni tamu mno likiwa limeiva tofauti na Bolibo lenyewe likiiva linakuwa tamu lakini si kama embe Dodo,uzuri wa Embe Bolibo likiwa bichi ni tamu mno na kama utalikata  kata vipande na kuliunga na chumvi na pilipili kwa mbali mno basi linakuwa tamu mno,ndio utamu wa embe huo.

Mbeya City leo ni kama Embe Bolibo ambalo msimu huu limechukua nafasi ya tatu ikiwa nyuma Azam Fc wana lambalamba na vijana wa Jangwani  Yanga Afrikan na Binslum ameingia kuchanganya Chumvi na pilipili ni utamu ulioje utaupata msimu ujao, nasema karibu  sana Binslum nyumbani, Mbeya ni moja kati mikoa inayoitwa Big Four yaani yenye chakula cha kutosha kulisha nchi nzima  lakini kizuri zaidi ikiwa imepakana na Nchi mbili kubwa yaani Malawi na Zambia ,Kampuni  ya Binslum Tryes co kupitia bidhaa yao ya betri za RB anasema namwaga milioni 360  mkataba mnono kabisa wa miaka miwili ni vipi soka lisipigwe Mbeya, na ni vipi Binslum asitengeneze biashara yake kiulaini katika nyanda hizo ni akili ndogo tu ambayo haiitaji uende Chuo Kikuu kujua kuwa Binslum ni mtu wa soka lakini ni mzuri mno kwenye Biashara,mbali ya kuwamwagia mpunga mbeya  ,Mkurugenzi wa Kampuni hiyo Binslum anasema anamwaga udhamini wake na pale Stand ya Shinyanga na Ndanda ya Mtwara  sehemu iliyopakana kwa karibu zaidi na Msumbiji unataka nini tena ni balaa,wasukuma na wamakonde wanacheka ,na Binslum sasa anafanya biashara yake Tanzania,Malawi,Zambia na Msumbiji safiiiii.


Mfadhili huyo anaonesha ni jinsi gani anavyokerwa na maendeleo ya soka ndani ya nchi hii ninawakumbuka Ramesh Pater Kaka  alivyokuwa akijitoa kwa ufadhili wa kuisaidia Tukuyu Star enzi hizo na akina Shafi Bora walivyokuwa wakiifadhili Majimaji ya Songea na kuzifanya timu hizo kuleta upinzani mkubwa katika soka letu hadi zote kuchukua ubingwa ndio leo anataka kufanya Binslum.

Binslum ambaye ni mzaliwa wa Tanga na akiwa na asili ya Tanga ambaye watu na wadau wa soka muda mwingi walimzoea na kumjua kuwa ni mfadhili wa Coastal Union  na shabiki wa kutupwa wa Liverpool lakini ghafla ameustua Ulimwengu na kuwaonesha yeye si tu mshabiki wa Tanga bali ni mpenzi halisi wa soka na kwamba soka lipo ndani ya damu yake hasa, na sasa anaelekeza nguvu zake sehemu tofauti na hadi nje ya mipaka ,nasema saafi saana Binslum.

Kampuni hiyo inayojihusisha na kuuza Matairi na Mabetri ya gari imeonesha changamoto kubwa  kwa kampuni zingine kujitokeza na kuzifadhili timu nyingine na hasa ndogondogo.

Ili soka angalau lipige  hatua tatu mbele inabidi tuwapate angalau akina Binsulum kumi hivi ,ili ligi iwe na mvuto zaidi na zile timu ambazo zenyewe zilijiwekea nadhiri kuwa ubingwa ni wao miaka yote basi zishike adabu, kwa mtazamo tu wangu binafsi wachezaji wa Tanzania wote wana uwezo unaofanana tofauti yao kubwa inakuja kwenye nguvu ya kiuchumi,zipo timu zinaingia katika ligi ya Vodacom hazina uhakika wa kula, kulala na hata kupata posho za siku,wachezaji wake wanacheza katika mazingira magumu mno kiasi cha kushawishiwa wakati mwingine kucheza chini ya kiwango iwe kwa bahati mbaya au kwa makusudi.
Lakini zipo timu chache mnoo zinacheza zikiwa na uhakika wa kula,kulala,posho na usafiri ni vipi wachezaji wake wasiwe katika kiwango kizuri muda mwingi kama sio muda wote ndio maana nasema soka letu linaitaji watu wazalendo kama akina Binslum.