Tayari jana ndio tumefikia tamati ya
michuano yetu ambayo kwa kweli kuanzia TFF na sisi wadau tulikuwa na shauku
kubwa ya kuhakikisha tunafuzu na kuingia ligi ya makundi kuumana na
Zambia,Carpe Verde na Niger na baadaye tuelekee Morocco mwakani na wale vijana
waelekee Benin lakini ndo tumekwama baad ya kuondolewa jana na Msumbiji kwa
magoli 2-1 na vijana wetu juzi kufungwa na Afrika ya kusini 4-0. Sasa macho na
masikio yetu turudi nyumbani tutengeneze mpira
TFF kupitia msemaji wake Boniface
Wambura imetutangazia kuwa ratiba ya ligi itatoka mwezi mmoja kabla yaani Agost
20 tayari itakuwa uwanjani na kila timu itajua inaanza wapi na nani ili
ijipange vizuri safi sana kwa hilo,Uongozi uliopita uliokuwa chini ya Leodgar
Shilla Tenga ulifanya mambo mengi mazuri ambayo kimsingi ni lazima yaigwe na
kuenziwa,iliweka utawala safi wa kujua nani anawajibika kwa hili na nani
anawajibika kwa lile,ilikuwa sio rahisi Tenga kumshika ubaya kwa kuwa mambo
yote aliyaacha kwa watendaji wake,wakati mwingine ni safi ingawa wakati
mwingine ni tatizo.
Katika jambo ambalo mwandishi wa makala
hii alikuwa akilipigia kelele kila kukicha ni mfumo wa ligi,jambo ambalo
lilimweka mbali mno na utawala uliopita na kumuona msaliti na kutompa nafasi
yeyote ya kusogea pale alipo katika taaluma yake na kuwaacha wadogo zake
wakipaa kila kukicha.
Katika mengi mazuri waliyoyafanya moja
la mfumo wa ligi kwangu mimi ilikuwa ni tatizo na naamini ndio limetufikisha
hapa tulipo,Mkurugenzi wa Ufundi wakati ule jambo la kwanza kabisa akaua ligi
zote za chini na kuanzisha ligi moja tu ya TFF ufa wa kwanza mbaya ambao
sikuukubali hadi leo ,Tenga kwa kuwaamini mno watendaji wake akaubariki,mwaka
2007 ikachezwa ligi ndogo ya kubadili mfumo ili tuwaige watawala wetu
waliotutawala yaani Waingereza kuanza ligi mwezi wa nane na kumaliza watano
safi sana wote tulipongeza tukasubiri utekelezaji,hapo ndio ilikuwa ni
kichekesho wenye kuona kwa jicho tukapiga kelele,wanaume wale walifumba macho
na masikio yao hadi wanaondoka madarakani waliacha ligi ya miezi sita inachezwa
na miezi sita wachezaji wamelala majumbani kwao na mishahara wakilipwa.
Ligi imekuwa ikianza mwezi agost
mwishoni na mwezi wa novembar mosi inasimama hadi mwezi march au February
mwishoni na ikifika April ligi imekwisha ukiangalia hapo mchezaji anakuwa
uwanjani kwa muda wa miezi isiyozidi sita halafu tunajidanganya kuwa tunaiga
mfumo wa Uingereza ambao wenyewe wakianza ligi Agost hawasimami hata iwe x mass
hadi mwezi wa tano tarehe 15 na wakiwa wamecheza mechi za ligi 38 achilia makombe mengi yapo katikati hapo,ndio
maana katika hilo nilipiga mno kelele na adhabu yake niliipata lakini bora iwe
hivyo kwa maslai ya Taifa.
Uongozi mpya ulioingia madarakani chini
ya Jamal Emil Malinzi ulipoingia madarakani uliunda kamati zake nyingi
mnoo,mojawapo ya kamati iliyonivutia ni ile ya kutengeneza mfumo wa ligi na
ikiongozwa na Profesa Mshindo Msola,haraka mno nilipiga hodi ofisini Msola nikimuonesha kukerwa kwangu na mfumo
uliopita na nilikuwa na kitabu changu cha zamani kidogo nilimuonesha mfumo wa
ligi na ratiba za ligi kuanzia ligi daraja la pili hadi ligi ya Muungano za
mwaka 1986-1990 jinsi wachezaji wetu
walivyokuwa wakicheza mechi nyingi na muda mrefu jambo ambalo wachezaji
wetu leo wamelikosa,ndio maana nasema
naisubiri kwa hamu ratiba hiyo kama itakuwa kama ile iliyopita basi soka
litazidi kwenda kuzimuu.
FIFA wanasema ili mchezaji afikie
kiwango cha kimataifa yaani cha ushindani ni lazima acheze mechi zisizopungua
40 kwa msimu mmoja sasa ni lazima tukae tujiulize wachezaji wetu wanacheza
mechi ngapi,kama atacheza mechi zote za ligi kwa muda wa miezi hiyo sita
atacheza mechi 26 tu ,na kama yupo timu ya Taifa ataenda akiwa hajafikia
malengo ya soka lenyewe pungufu mechi 14 atakuwa ni kichekesho tu
Nilimwonesha Kaka yangu Mshindo Msola
ligi ya miaka ikichezwa kwa muda miezi tisa bila kusimama,na kama timu ya Taifa
ina michuano ligi yetu inaendelea kasoro ile timu itakayokuwa na wachezaji
zaidi ya watatu,ratiba inaonesha ikiisha ligi yetu inakuja ligi ya
Muungano,halafu Taifa Cup yaani michuano
ya mikoa ambayo haiwazuii wachezaji wa ligi kuu kucheza na mwisho timu bingwa
inakwenda katika mashindano ya klabu bingwa ya vilabu katika ukanda wetu wa
Afrika Mashariki na ya Kati.
Nilimdhibitishia Msola itakapofika suala
la kujadili mfumo kama unadhani mawazo yangu ni sahihi niite kwenye kamati
kimyakimya na siitaja posho yeyote nije nitoe mawazo yangu tunahitaji ligi bora
na si bora ligi.
Inasikitisha leo Haruna Nyonzima
,Emanuel Okwi,Owino,Musoti,Kiiza na wengineo wa nje wanakaa muda mrefu katika
nchi zao tofauti na sisi kwa Mbwana Samata na Thomas Ulimwengu ambao ni nadra
mno kuwaona nyumbani maana Samata me ni jirani yangu simuoni kabisa nyumbani.
Timu zinaingia mikataba mikubwa na
minono kwa wachezaji wao lakini matumizi yao ni kipindi kifupi mno,haingii
akilini uwe na kampuni na umwajiri mfanyakazi wako afanye kazi miezi sita na
sita kalala kwa mkewe au mumewe halafu umlipe mshahara wa mwaka mzima utegemee
kupata faida haiwezekani,ndio maana leo nasema yapo mazuri mengi mno
aliyoyafanya Tenga ambayo Malinzi inabidi ayaendeleze lakini kwangu mimi hili
kama TFF hii italiendeleza me natoa Shilingi yangu.