“Uaminifu unajengwa na
‘consistency’(msimamo)” hayo ni maneno
ya mwanasiasa nguli wa marekani ambaye ni Gavana wa 74 wa visiwa vya rhodes
bwana Lincoln Chafee.Usemi wa bwana chamfee unanifanya niwakumbuke wachezaji
waliokosa kitu kinachoitwa ‘consistency’.Wachezaji hao wengi vipaji sana ila hawavumi kwa muda mrefu.
Desemba
2007 wakati wa mechi ya Almeria na Barcelona washabiki wa Barcelona walidiriki
kumzomea Ronaldinho Gaucho.Kuna baadhi ya watu walishangaa,Huku wengine
wakijiuliza washabiki hao wametoa wapi ujasiri wa kumzomea Ronaldinho
Gaucho.Ronaldinho ambaye amewapa makombe ya ligi mawili,na kombe la klabu
bingwa ulaya moja,Tena akiwa kwenye kiwango cha hali ya juu.Bado wengi
walijiuliza Hawa washabiki wa Barcelona wanawaza nini mpaka kumzomea mchezaji
bora wa Dunia mara mbili mfululizo kwa miaka miwili iliyopita.Jibu ni kuwa
Ronaldinho alikosa ‘consistency’.Kwenye umri wa miaka 27 aliokua nao bado
alikuwa na uwezo wa kuwapa vitu zaidi mashabiki wa Barcelona.Ila hali haikua
hivyo kama mashabiki walivyotarajia.Wazungu wanasema “too much expectation
result to greater disappointment”.Mashabiki wa Barcelona bado walikua na
matarajio makubwa kwa Ronaldinho lakini akawakatisha tama kwa kiwango chake wasichokitarajia.Kadiri
siku zilivyoenda kiwango cha Ronaldinho kilishuka jambo lililopelekea
kufungashiwa virago vyake,na huo ukawa mwisho wa Ronaldinho ndani ya uzi wa
Barcelona.
Mchekeshaji
maarufu Duniani raia wa mexico Louis Ck
aliwai sema “Kama ukifanya kazi kwa bidii na kutumia muda na nguvu nyingi
kwenye kitu unachokifanya na kwa mwendelezo wenye msimamo(‘consistency’) lazima
utapata matokeo mazuri kwenye hicho unachokifanya”.Nikiangalia wachezaji wengi
wanaocheza soka la bongo hasa wale wanaopata majina kidogo wanakua na tabia
kama za Ronaldinho.Wengi hawataki kufuata kauli ya Louis Ck.Wengi wamekosa vitu
hivyo viwili yaani bidii na ‘consistency’.Kila nikimuangalia Uhuru seleman
lazima nimkumbuke Ck.Uhuru seleman amekosa ‘consistency’ jambo linalohatarisha
maisha yake ya soka.Wana Simba na Watanzania wengi walikua na matarajio makubwa
kutoka kwenye miguu iliyobarikiwa ya Uhuru seleman.Ni mmoja wa wachezaji wenye
vipaji maridhawa Tanzania lakini kiwango chake kimekua kikiporomoka kila
unapomuona.Wakati naangalia mechi ya Coastal union na Simba niliona kiwango
chake kibovu kabisa tangu nianze kumshuhudia.Bila shaka Uhuru seleman hafanyi
mazoezi kwa bidii,Siku si nyingi mashabiki wa Simba watamkataa uhuru kwa kuanza
kumzomea.Uhuru akiendelea hivyo maisha yake ndani ya Simba yatakua mafupi mno
kama ya Ronaldinho ndani ya Barcelona.
Upande wa pili wa shilingi wana habari mpya
inayoitwa Jaja.Ukipita kwenye meza za magazeti bila kulikuta jina la jaja basi
ujue ilo gazeti limepitwa na wakati.Kwa sasa jaja ni kipenzi cha mashabiki wa
Yanga.Jaja anapendwa kwasababu amewapa mashabiki wa Yanga walichokihitaji kwa
muda stahiki.Washabiki wa Yanga wengi walikua wana kidonda cha kuondoka kwa
Emmanuel Okwi.Tena mbaya zaidi kwenda kwa mahasimu wao wakubwa.Mashabiki wa
Yanga walihitaji mtu atakayewaaminisha kuwa Okwi si lolote kwao.Walikua
wanahitaji faraja kuliko kitu chochote kwa muda huo.Na jaja hakufanya makosa
akawafariji.Akawapa raha zilizowafanya wamsahau Emmanuel Okwi kwa muda.Mabao
mawili aliyoyafunga dhidi ya Azam
yalikua dawa kwa ugonjwa uliokua ukiwasumbua
mashabiki wa yanga kwa wakati huo.
Ila
bado nawaza,Je jaja anaweza kuendeleza kiwango alichokionesha kwenye mechi ya
Azam?.Hapa ndipo nnapomkumbuka Said Bahanuzi.Baada ya Yanga kufungwa goli 5 na
Simba aliwapa mashabiki bao 6 kwenye kombe la Kagame,Mabao yake yaliiwezesha
yanga kuchukua kombe la kagame na kusahau kipigo cha bao 5 walichokipokea miezi
miwili kabla.Bahanuzi alijaa kwenye mioyo ya washabiki wa Yanga,Mpaka wakafikia
kumuita habari ya mjini na wengine wakamuita Spider Man.Lakini leo hii hakuna
mshabiki wa yanga anayemuelewa Bahanuzi,kwasababu ya kukosa ‘consistency’.
Jaja
najua hujui Kiswahili,Ila nna imani Ngasa,Kaseja na Yondani watakupa tafsiri ya
hili muhimu nnalotaka kukwambia. Jaja inabidi ujue nini wayanga wanataka kwa muda huu. Wanayanga
wanataka kombe la ligi kuu ya Vodacom .Ili yanga wapate kombe la ligi kuu ya
Vodacom wanahitaji mabao ya kutosha kutoka kwako.Jaja inabidi uwe na kiwango
kisichopanda na kushuka yaani uwe
na‘consistency’ Ukiwa na kiwango kisichobadilika utafunga magoli na kuwapa
yanga ubingwa.Hapo utakua umeshinda mioyo ya wanajangwani.Wana Yanga
hawatakuelewa kwa sababu ulifunga magoli mawili dhidi ya azam ila watakuelewa
kama utaendelea kufanya ulichokifanya dhidi ya azam.
Lakini
Jaja kwa ulichoanza kukionyesha kwenye Uwanja wa Jamhuri unaanza kunipa mashaka,bado najiuliza kama kweli yale magoli yako uliyofunga dhidi
ya azam ndio kiwango chako halisi au uliamka vizuri tu siku hiyo.Bwana Jaja
naomba ufanye hili kwa usalama wako.Mwenzako Said Bahanuzi asingekua Mtanzani
angeshatupiwa virago vyake zamani sana.Naye Alikuwa Habari ya Mjini kama wewe.Usipokua
makini na wewe utakuwa habari ya mjini
kwa miezi miwili kama alivyokua
Bahanuzi.Usipowapa wana yanga wanachohitaji watakuzomea,hawatokupenda
tena na matokeo yake utaenda uwanja wa ndege kuelekea kwenu brazil bila
kusindikizwa na vuvuzela za yanga bomba.
Na allen kaijage
0655106767
kaijagejr@gmail.com