Hakika nyakati zinapita na muda
unakwenda, majira yanabadilika na miaka inakwenda au kwa namna nyingine umri
wako na wangu unakua. Umri unavyozidi kwenda basi uwezo na utambuzi wa vitu au uelewa wa mambo
unakua kwa haraka sana ila kama tu utaruhusu mwili ukue pamoja na akili. Malezi
uanzia kwa wazazi wetu pamoja na jamaa zetu ambao wanatulea huku katika jamii
zetu. Kwa nyakati zetu tulielekezwa vitu vingi sana japo siyo vyote kwa mfano
kuweza kukadiria muda kwa kulitazama jua au kuweza kujua mahala au uelekeo yani
kaskazini au kusini kwa kuangalia nyota wakati wa usiku. Naamini haya yalikuwa
baadhi ya mafundisho kutoka kwenye simulizi za mababu zetu au nyanya wetu.
Kwa vijana wa enzi za analojia ni
tofauti sana na dijitali, kwasababu vijana wa analojia wanajua nini maana ya
kutandika na kutandua mkeka chini ya mti au miti iliopo mbele ya nyumba yao
hasahasa wakikimbilia nafasi za mbele kusikiliza simulizi za mababu yani
hadithi zenye mafundisho mengi sana kama methali, vitendawili na nahau au
misemo mbalimbali. Subira yavuta kheri, au mvumilivu hula mbivu, vipi
unazikumbuka hizi. Najua unatabasamu, ndio haya ni baadhi ya maneno ya wahenga
tu.
Wahenga wanawashangaa sana viongozi na
baadhi ya walimu wa mpira wa Tanzania na huku wakijiuliza maswali mengi sana
kama kweli hawa walimu walitandika na kutandua mikeka ili kusikiliza simulizi
zao, najua wanaumia sana na mioyo yao inanung’unika sana wakihofia kwamba hawa
walimu na viongozi wa soka letu ni kweli wanakumbuka simulizi zao au
wanazikumbuka lakini wameamua kupuuzia tu. Na maswali yao mengi ni kwamba
, hata kama wanazikumbuka kwanini basi
hawatumii utaalamu wa kusoma muda kwa kuangalia jua au kuishi kwa kulingana na
nahau na misemo yao yenye mafundisho.
Kipenga cha ligi ya Tanzania bara
kipeshapulizwa kuangalia ni nani atakabidhiwa kombe na wanalambalamba yani Azam
Fc au wanalambalamba hao watajitetea na kulitunza tena kombe lao katika mifuko
yao ya Azam. Viongozi wa vilabu tofauti vya ligi yetu wanashindwa kabisa
kutofautisha uzoefu, ubunifu na ujuaji, na matokeo yake wanapingana na methali
ya “subira yavuta kheri au “mvumilivu hula mbivu” na hapo ndipo
wanapowakasilisha wazee wa simulizi za mikeka na kuamua kuitupa au kuificha
mbali mikeka yao. Matokeo ya haya yote pamoja na kukosa somo la kutofautisha
vitu hivyo vitatu wanaamua kuchagua au kubadili makocha wa vilabu vyao kwa
kusikiliza ufundi wa mdomoni au ujuaji na kuacha kuangalia swala la ubunifu na
uzoefu.
Msimu wa ligi ilyopita yani msimu
uliopita tulishudia kufukuzwa au wenyewe wanaita kubadili kwa makocha wa timu
kumi na mbili tofauti za ligi yetu na kuziacha timu mbili tu ambazo wahenga
wanaamini viongozi wa timu hizo ndio waliotandika mikeka wakati wa umri wao
nazo ni Mtibwa Sugar na Mbeya City na walimu wao Juma Mwambusi na Meckie
Mexime. Viongozi wa timu hizi walikuwa na staha na heshima na kuelewa kuwa kila
kitu kizuri kinahitaji muda na nafasi nzuri bila msukumo wa kishabiki au
maslahi binafsi, naamini wote tulishuhudia viwango vya timu hizi mbili japo
hazikufanikiwa kuchukua ubingwa.
Hivi kwanini viongozi wa vilabu
vya Tanzania wasimuangalie kocha mzuri kwa kutazama mbinu zake, uwezo wake na
ubunifu wake katika mpira na waache kuangalia uwezo wa kocha kwa kutazama au
kwa kusikiliza mazungumzo yake hasa akielezea mfumo wake wa uwanjani. Kwa
muelekeo wa hivi sasa hata wewe ukiwa muongeaji mzuri na unamfahamu hata mjumbe
mmojawapo katika kilabu husika basi utapewa nafasi ya kuwa kocha wa timu hiyo.
Ifike wakati viongozi wa vilbu tofauti wawe na subira na heshima kwa makocha wa
vilabu vyao kwa kuwaamini na kuwapa motisha mi naamini
watashinda tu japo katika ushindani lazima kila nafasi iwe na mwenyewe kuanzia mshindi
mpaka anayeshuka daraja.
Umefika wakati walimu wa soka letu na
viongozi wa vilabu vyetu kutandikiwa mkeka na kusikiliza simulizi za mababu
zetu ili wajikumbushe busara na maneno yenye mashiko ili wavitumie katika mpira
na kuacha kuwanyayasa makocha kwa kujifanya wao ni wajuaji. Wafundishwe
kujipenda na kujijali wao kwanza na siyo kuwapa nafasi kwa kiasi kikubwa
makocha wa kigeni kuja kufundisha vilabu vyao kwa hofu zao tu, wakati kuna watu
kama Mbwana Makata, Abdallah Kibaden ,Hemedy Morocco na wengine wengi ambao
wakifanya masomo kidogo, na elimu nzuri kwa nadharia ya vitendo wanaweza kuwa
walimu wazuri sana na wakutumainiwa hasa tu wakiaminiwa. Kilichobaki ni kuifuma
mikeka na kuandaa vipaza sauti tayari kwa simulizi au hadithi za wahenga.
Na,
Kelvin
Kiimbila Jr
0719580495