Kama Kuna swali gumu na lisilo na Jibu sahihi miongoni mwa maswali mengi katika viwanja vya soka basi ni lile linalohusisha neno kipaji. Kila nikimtizama Angel Di Maria Kisha nikatupa jicho mahala alipo Downing baadae nikamtizama Yaya Toure Kisha nikaona anachofanya Lucas roho inauma zaidi. Hata hivyo ndio soka, linakupa Majibu na maswali tofauti. Wakati unawaza uwezo wa Yaya Toure unajiuliza ni vipi anadhibitiwa vilivyo na yule Charlie Adam wa Stoke City wakati katika karatasi hafiki nusu ya uwezo wake? Ndio maana Siwezi kumshangaa James Pinkerton alivyyowahi kusema kuwa HAKUNA LILILOSAWA KATIKA HII DUNIA AMBAYO HAIPO SAWA.Alikuwa sahihi zaidi, dunia haipo sawa, watu hatupo sawa hata vipawa havipo sawa pia. Bahati mbaya tu hatuna namna Mara nyingine inabidi uviweke visivyo sawa vifanye kitu kimoja. Ni kama kushudia Messi na Sanogo wakiwa watu wa nafasi moja uwanjani katika timu kubwa mbili tofauti.
Umewaza Ubingwa wa Premier League msimu huu? Kwakua dunia haipo sawa
kama James Pinkerton alivyosema si ajabu hata mashabiki wa Liverpool
baadhi wapo ambao bado wanaofikiria na kuamini kuwa wanaweza kupata
ubingwa. Ingawa kwa wale wanaoshika kalamu na karatasi vyema wana imani
Mourinho anayo nafasi kubwa zaidi ya mtu yeyote, unahitaji roho ya Daudi
yule wa Goliath kulipinga hili yaani roho ngumu na ya kijasiri kweli.
Nipo nauwaza ubingwa wa Chelsea, lakini kwa namna tofauti kidogo.
Najiuliza kama ikitokea nani atatizamwa kama mfalme? Nani ataimbwa Sana
pale Stamford bridge? Nani atayarithi yale mabango mazuri ya Super
Frankie Lampard kule jukwaani? Baadae nawaza nani atakuwa kipenzi cha
Abramovich? Hapana shaka wa kwanza atakuwa Mourinho mwenyewe, na kwa
ubinadamu mwingine atakuwa Diego Costa Kisha Cesc Fabregas. Kuna Tatizo
hapa, yule fundi wao Eden Hazard sio ajabu akawa nyuma ya Nemanja Matic.
Unajua kwanini? Sitoshangaa Sana ikitokea hivyo na Jibu ni rahisi tu,
dunia haipo sawa kwa kiasi kikubwa hivyo na Hazard hajakaa sawa. Kwa
lugha ya kitaalamu katika soka Hazard anakosa kitu kinaitwa FOOTBALL
MATURITY, yaani anakosa ukomavu wa soka. Ukomavu unaanzia katika
uwezo,Kisha malengo baadae maamuzi. Hapa akili inabidi iwe imeiva kweli.
Hazard ana uwezo, malengo lakini analo tatizo la maamuzi. Maamuzi yake
huwa sahihi Sana pale anapopiga penalti kuliko anapokuwa anamiliki mpira
ndani ya uwanja. Na hii ndio sababu inayomweka nyuma ya wachezaji wengi
katika mtiririko wa heshima, tuzo na ubora.
Hakuna uhalisia wowote wa uwezo wa Sterling juu ya Hazard, usiwaze
kuhusu Mata dhidi ya Hazard, kama ni kipaji Hazard anawekwa ukurasa
mmoja na Angel Di Maria. Na pengine ndio mchezaji mwenye mbinu nyingi
zaidi na umaridadi wa kipekee awapo uwanjani kuliko mchezaji mwingine
yoyote Ligi ya Uingereza. Lakini anao huo ugonjwa tu unaoitwa ukomavu.
Kwa mchezaji Kuna umri ukifika ama kipindi kikifika unaacha baadhi ya
mambo na kufanya vile vitu vya msingi zaidi, unaacha kupiga chenga
wachezaji wanne, unaacha kukimbizana na mpira kwenye msitu wa watu kwa
sekunde 50, unapunguza mchezo wa kwenye kioo ule wa Adnan Januzaj, huu
ni mchezo wa makinda bora wanaochipukia katika kuvutia wawekezaji ambao
ni timu kubwa. Katika kipindi hiki we unajifunza na unajikita katika
kujiweka katika nafasi sahihi na katika muda sahih. Unaacha kupigana
vikumbo na akina Shawcross au Koscielny unajifunza kucheza pembeni mwa
mabega Yao. Maana yake kwa lugha nyepesi unaanza kujifunza kucheza na
kipa na sio mabeki yaani ujifunze kufunga, Hazard Ana shida hapa,
anaumwa hapa na amelala hapa. Hazard analo tatizo la kutoweza kuwa
muhimili wa awali kabisa wa timu, atakupa kile unachotaka kama tu Kuna
mtu mwingine wa kufanya baadhi ya majukumu ambayo kimsingi alitakiwa
ayafanye yeye. Kwa Hilo huwezi shangaa kwanini Juan Mata aliweza kuwa
mchezaji bora Mara mbili wa chelsea mbele yake. Kwa hilo hapana shaka
Chelsea wangeweza kuwa mabingwa msimu uliopita kama wangekuwa na nguzo
nyingine pembeni yake achilia mbali tuzo ya mchezaji bora anayechipukia
aliyopewa ambayo ninaamini kwake ilichelewa na alitakiwa kuipata misimu
miwili nyuma. Soka la sasa linampa ugumu Hazard, mbio, chenga, na Kanzu
na magoli machache na assist kiasi haviwezi kukupa Ballon D'or katika
Ulimwengu huu ambao Diego Costa na Suarez wanafunga goli 30 peke Yao,
katika dunia hii ambayo wachezaji wa pembeni wenye uwezo wanatakiwa
kufunga kwa kiasi kikubwa. Hapa ndipo mabadiliko yake yanatakiwa. Kwa
wachezaji wa kariba yake unahitaji uwezo mkubwa wa kufunga ili uwe na
uelekeo wa kuwa Mchezaji bora wa dunia. Roho inaniuma maana naona mwenye
uelekeo huo katika kundi la kina Hazard ni Neymar. Huyu ndio anayekomaa
vizuri pamoja na akina Bale na James Rodriguez. Hata Ubelgji
walishindwa hapa, alichotakiwa kufanya Hazard alikifanya De Bryune,
mchezaji tusiemfikiria huko juu. Dunia haipo sawa kweli, ndio maana
Hazard anaiwaza Ballon D'Or pasipo kubadili maamuzi. Sio maamuzi mengine
Bali ni yale maamuzi unapokuwa mbele ya goli. AJUE KUFUNGA TU.
Vinginevyo tutaendelea kumsujudia Alexis Sanchez kama mchezaji wa Pluto.
Mi kwangu Hazard bado mtoto sijui kwako wewe, ila mi naamini hajakomaa.
Acha niwaze kuwa atabadilika,ingawa ananipa wasiwasi kama ataweza kuwa
mshindi wa Ballon D'OR , anaweza hasibadilike si unajua hakuna lililo
sawa katika dunia hii isiyo sawa na ndio maana wengine tunaenda mbali na
kumfananisha na Ronaldo Cristian huwa natamani kulia lakini nahairisha
kila nikimkumbuka James Pinkerton, kweli hakuna lililo sawa katika dunia
hii isiyo sawa lakini natamani kuiona suti ya Hazard miaka fulani akiwa
miongoni mwa watatu wanaotakiwa kushinda Ballon D' Or.
Ahsanteni
By Nicasius Coutinho Suso
Ahsanteni
By Nicasius Coutinho Suso