Mshambuliaji
wa Kagera Sugar Rashid Mandawa amesema kuwa ataendelea kula sahani moja na
Mrundi Didier Kavumbagu katika kuwania zawadi ya mfungaji bora wa Ligi Kuu
msimu huu.
Mandawa
aliye kwenye kiwango cha juu hivi sasa, ameshafunga mabao nane wakati Kavumbagu
anayeongoza ameshatumbukiza nyavuni mabao tisa jambo linalozidi kuleta
ushindani baina yao.
Akizungumza
na Mwandishi wetu jana, Mandawa alisema lengo lake ni kuibuka mfungaji bora wa
ligi kuu na pia kuisaidia Kagera Sugar imalize ikiwa katika nafasi nzuri kwenye
msimamo wa ligi hiyo.
“Kavumbagu
ni mshambuliaji mzuri anayezidi kunihamasisha mimi kufanya vizuri. Nataka
nilipe fadhila kwa timu yangu ya Kagera ninataka imalize ligi ikiwa kwenye
nafasi za juu,” alisema Mandawa
Mandawa ni
miongoni mwa washambuliaji wazawa ambao wamekuwa kwenye kiwango cha juu kwa
kuzifumania nyavu na kuleta ushindani kwa wageni ambao walikuwa wakitawala.