MWADUI IMEPANDA SHUGHURI IMEIVA
Nimesoma Mwadui,nimekulia Mwadui nimecheza mpira Mwadui
naijua vizuri Mwadui ,ukifika Mkoani Shinyanga unatoka kidogo nje ya mji kama
unaenda Mwanza unapita vitongoji vya Korandoto na Maganzo mbele kama mita tano
hivi unapinda barabara upande wa kulia unakutana na geti kubwa la kuingia katika
Mgodi wa Mwadui unaojishugulisha na kuchimba Almasi, ni Mgodi ambao bado ndungu zetu wa Afrika kusini bado
wana hisa yao katika Mgodi huo ambao ulivumbuliwa Williamson.
Mwadui ni eneo ambalo mambo unayo yasikia kule Ulaya
yalikuwepo Mwadui wakati nikiishi kule miaka ya 70 hadi ya 80 ,ilikuwa tunaishi
maisha kama hauko Tanzania, sina hakika na leo ,wachezaji wa Mwadui enzi hizo
tulikuwa tunalelewa kama tupo Ulaya katika Hostel ya Uhuru , Mwadui ndio timu pekee
miaka ile ilikuwa ikisafiri kwa Ndege kwenda sehemu yeyote kucheza soka,ina
Super Market kubwa mno sijapata kuona enzi zile, ni sehemu pekee miaka ile
matumizi ya pesa ya cash ilikuwa si muhimu kama ilivyo leo Mitandao ya tigo
pesa na M pesa inavyotufanya tusitembee na hela,ina viwanja bora na vingi vya
kufanyia mazoezi kuanzia vile vya maeneo ya Posta hadi Compaund,wachezaji
walikuwa hawana kabisa matatizo ya kula ,kulala, matibabu wala vifaa.
Kwa mazingira hayo Mwadui mbali ya kutoa timu nzuri na wachezaji wenye kuleta upinzani mkubwa katika
soka letu miaka ile bado iliweza kuibua kocha iliyepata kufundisha timu ya
Taifa akitokea Mwadui Mzee Elijah Kategile,ni moja kati ya makocha
waliotupeleka hadi kwenye Mataifa huru ya Afrika akishirikiana na Mh Joel
Bendera na Mohamedy Msomali ambayo hadi leo bado tunayatolea macho.,Mwadui
iliweza kuleta wachezaji katika timu ya Taifa kama akina Joseph Mbelwa maarufu
kama Bagina,Zuberi Kaiwanga,Hamis Kamaka,James Ngo’nga,Ahmedy Abasi ,David
Mwakalebela ,Justine Simfukwe na wengineo
Lakini Mwadui imewahi kuwa na wachezaji zaidi ya hao ambao
walikuwa maarufu na hawakucheza timu ya Taifa kama akina John Lega ,Rwemaho
Mkama, Benard Madale,Anko Shubetr,Chia Masonga,Wagadugu,Tostao,Ally Bushiri,Deus
Kapandila,Masolwa ,Yona Kiombo,Mkama Ntale,Aman Rashid,Ally Bushiri na wengine
wengi tu.
Chimbuko la wachezaji hao ni utaratibu mzuri wa mashindano
yao ya ndani ambayo yalikuwa yanashikrikisha timu za Idara kuanzia ile ya
Mji,Uhandisi,Uzalishaji ,Utawala hadi Almas na mgeni rasmi wa kukabidhi kombe
na zawadi alikuwa akitoka Afrika kusini na ndio ilikuwa chachu ya kupata
wachezaji wa kuunda timu ya Mwadui.
Leo Mwadui ile ninayoifahamu mimi kama ndio yenyewe ambayo
imepanda daraja chini ya kocha mwenye mbwembwe nyingi hapa nchini lakini pia
akiwa na mafanikio mazuri tu ya soka Jamuhuri Kiwhelu maarufu kama Julio,naamini kutakuwa na shughuri pevu msimu
ujao.
Kocha Jamuhuri Kiwhelu
ni moja kati ya makocha wazalendo wanaoujua vizuri mpira na mashindano
ya nyumbani kwetu,anamjua kila mtu aliye wa mpira na hata Yule anayejiita mtu
wa mpira,Julio ni mpambanaji ni mpenda sifa asiyekubali kushindwa lakini cha
zaidi ni msema ukweli na hafichi kutoa hisia zake hivyo hata kama kuna watukama
wanataka kumuharibia matokeo hatakaa kimya atapiga kelele tu na watu tutaona
kuwa hapana hapa Mwadui wanaonewa, Julio analijua soka letu.