Uongozi wa Simba umempiga kijembe Ofisa Habari na Mawasiliano wa Klabu ya Yanga Jerry Muro kuwa amewekwa kwenye nafasi hiyo kimakosa.
Kauli ya Simba imekuja kufuatia tamko lililotolewa na Jerry Muro kuwa yuko tayari kujiuzulu nafasi yake, ikiwa Simba haitopokonywa pointi tatu kutoka kwenye mechi ya Prisons baada ya kumtumia mshambuliaji Ibrahim Ajibu ambaye alikuwa na kadi tatu za njano.
Hata hivyo TFF sambamba na Bodi ya Ligi vimeshatolea ufafanuzi suala hilo kwa kudai kuwa Ajibu alikuwa huru kuichezea Simba ambayo ilimuombea ruhusa ya kucheza mechi hiyo kutokana na mabadiliko ya kanuni yaliyofanywa na kamati ya utendaji mnamo tarehe 8 mwezi Februari.
Akizungumza na moja ya vituo vya redio hapa jijini leo asubuhi, mjumbe wa kamati ya utendaji ya Simba Said Tulli, alisema kuwa Yanga walifanya makosa kumpa nafasi hiyo Muro ambaye hana ufahamu na mambo ya soka.
"Jerry Muro alishazoea kupiga picha Matrafiki na Polisi barabarani anataka kuleta mambo hayo kwenye mpira. Anatakiwa atulie na kujifunza mambo ya soka na asilete mambo ya kurekodi matrafiki wakipokea rushwa kwenye soka," alisema Tulli.
Kauli ya Tulli inaweza kuibua vita mpya kati yake na Muro ambaye tangu alipoajiriwa kushika nafasi hiyo, amekuwa misimamo mbalimbali inayozua gumzo kwenye medani ya soka hapa nchini.
Simba wamcharukia Jerry Muro
Info Post