Breaking News
Loading...
Friday, 27 April 2018

Info Post


TIMU inayoundwa na wachezaji chipukizi ya Tumbaku ya Morogoro leo iliwavua ubingwa wa michuano ya Kombe la Mei Mosi timu ya Geita Gold Mine (GGM) na kutinga hatua ya fainali baada ya kuwafunga magoli 4-1 katika mchezo wa kwanza wa nusu fainali uliofanyika kwenye uwanja wa Samora mkoani Iringa.
Tumbaku ambayo haijapoteza mchezo tangu ilipoanza hatua ya makundi ikiwa kundi A na GGM ikiwa kundi B ilianza kupata bao lake la kwanza kupitia kwa mshambuliaji wake Kelvin Makamba aliyepiga shuti kali nje ya 18 katika dakika ya pili.
GGM walisawazisha katika dakika ya 44 kwa kichwa kilichopigwa na Oswald Binamungu baada ya kupata pasi ya Ferdinand Makaranga.

Tumbaku waliongeza bao la pili katika dakika ya 51kupitia kwa mshambuliaji wake Issa Simbaliane aliyepiga mpira wa faulu uliokwenda moja kwa moja golini, huku bao la tatu lilipachikwa kimiani katika dakika ya 62 baada ya Emmanuel Mwakibinga kuunganisha kwa kichwa kona iliyochongwa na Idd Likasi.
Kiungo Idrisa Magongo alifunga kitabu cha magoli katika dakika ya 79 kwa kufunga bao la nne.
Hatahivyo, Katibu mkuu wa timu ya GGM, Wilhemin Bayanga pamoja na kukiri mchezo ulikuwa mkali na mzuri lakini wameikatia rufaa timu nzima ya Tumbaku kwa madai wamechezesha mamluki.

Katika mchezo mwingine wa nusu fainali timu ya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) imeingia fainali baada ya kuifunga timu ngumu ya Uchukuzi kwa magoli 2-1. Uchukuzi ndio walikuwa wa kwanza kupachika bao katika dakika ya 67 kupitia kwa Omary Kitambo.
Tanesco walisawazisha kwa njia ya penati iliyotolewa na mwamuzi Winfred Fyataga, katika dakika ya 70 na Seleman Ismail baada ya kipa Willy Barton kumchezea madhambi  Gossage Mtumwa. Bao la ushindi la Tanesco lilifungwa na Fortunatus Mgimba katika dakika ya 76 baada ya kipa Barton kuusukumiza mpira wa kona uliochongwa na mfungaji.
Kocha Mkuu wa Tanesco, Fidelis Almas amekiri leo atakuwa na kibarua kipevu kutokana na Tambuku kutokana na wachezaji wake kuwa chipukizi zaidi.

Ninajua mechi itakuwa kali lakini tumejiandaa kukabiliana na Tumbaku kwani tunawajua kutokana na kuwaona mara kadhaa wakiwa wanacheza na tulikuwa kundi moja, alisema Almas.
Wakati huo huo, timu ya Uchukuzi imeongeza kikombe baada ya kushinda Mzee Omari Said kuibuka bingwa katika mchezo wa bao uliofanyika kwenye ukumbi wa Manispaa Iringa. Ushindi wa pili ulichukuliwa na Suleiman Chitanda wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Shaaba Kidangala wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) aliibuka wa tatu