Breaking News
Loading...
Friday, 27 April 2018

Info Post


Mkuu wa Habari na Mawasiliano wa Klabu ya Simba, Haji Manara amewaasa waandishi wa habari na wadau wa soka nchini kuacha kutumia neno 'Mahasimu' wakimaanisha Simba na Yanga, badala yake ameshauri litumike neno 'Wapinzani' au 'Watani' wa jadi.

Amesema neno ‘Mahasimu’ linawafanya mashabiki wa soka nchini waamini kuwa Simba na Yanga ni maadui jambo linaloweza kuwafanya wajenge chuki kati ya mashabiki wa Simba na Yanga.

Nikimsikia mwandishi anatumia neno ‘Mahasimu’, klabu ya Simba itatangaza uadui na yeye, tumieni neno wapinzani wa jadi au watani wa jadi,” amesisitiza Manara.

Manara ametoa ombi hilo muda mfupi uliopita wakati akizungumza na wanahabari kuhusu maandalizi ya mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, utakaopigwa Jumapili wiki hii kwenye Dimba la Taifa Dar es Salaam dhidi ya Yanga, ambao utakuwa mbashara Azam Sports 2.

Amesema kikosi chao tayari kimerejea jijini Dar es Salaam kutoka Morogoro, na kiko tayari kwa mpambano huo.

Aidha Manara amewaasa waamuzi wa mchezo huo kutumia sheria 17 za soka na kuchezesha kwa haki ili kuepusha malalamiko yasiyo ya lazima.