Breaking News
Loading...
Tuesday, 24 April 2018

Info Post



Kocha Mwinyi Zahera kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), yupo mjini Dar es Salaam kwa ajili ya mipango ya kujiunga na klabu ya Yanga.

Taarifa kutoka Yanga zinasema kwamba kocha huyo anatarajiwa kuondoka leo Dar es Salaam kwenda Morogoro ambako kikosi cha timu hiyo kimeweka kambi kujiandaa na mchezo ujao wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya mahasimu, Simba SC.

Mwinyi alikuwa kwenye benchi la Ufundi la timu ya taifa ya DRC, The Leopard na uzoefu wa kufundisha soka hadi Ulaya, nchini Ufaransa.

Hii inamaanisha Yanga imeamua kuachana moja kwa moja na kocha wake, George Lwandamina aliyeondoka wiki mbili zilizopita kurejea kwao, Zambia kukamilisha mipango ya kujiunga tena na klabu yake ya zamani, Zesco United. 
Na tangu aondoke, klabu imebaki chini ya makocha waliokuwa wasaidizi wake, Mzambia mwenzake, Noel Mwandila na wazawa, Nsajigwa Shadrack na Juma Pondamali ambaye ni kocha wa makipa.

Kwa sasa kikosi cha Yanga kipo kambini mjini Morogoro kikijiandaa na mchezo dhidi ya Simba Jumapili Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam.