Breaking News
Loading...
Wednesday, 25 April 2018

Info Post


Mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga SC wamethibitisha kupata kocha mpya ambaye atarithi mikoba ya aliyekuwa kocha wao, Mzambia George Lwandamina.

Kocha huyo ni Zahera Mwinyi kutoka nchini DRC lakini ana uraia wa Ufaransa, na tayari amekwishatua jijini Dar es Salaam kujiunga na timu hiyo tangu jana Aprili 24, 2018.

Mkuu wa Habari na Mawasiliano wa Yanga Dismas Ten, amesema kocha huyo bado anaendelea na mazungumzo na Katibu Mkuu wao Boniface Mkwasa, na baada ya hapo kila kitu kitawekwa hadharini ikiwa ni pamoja na muda wa mkataba atakaopewa.

Licha ya Yanga kumuhitaji kocha wa aina hiyo kutokana na kukabiliwa na michuano ya Kombe la Shirikisho Barani, mtihani wake wa kwanza utakuwa ni kutetea taji la Ligi Kuu Tanzania (VPL) kwa kuanza na mchezo dhidi ya watani zao wa jadi, Simba utakaopigwa Aprili 29 mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Akizungumza baada ya kuwasili nchini, kocha Zahera amesema mechi dhidi ya Simba haimtishi kwani ana uzoefu wa kupambana katika mechi ngumu za aina hiyo, hivyo kwa upande wake hakutakuwa na jipya.

Kabla ya kujiunga na Yanga, Zahera alikuwa ni kocha msaidizi wa timu ya Taifa ya DRC, lakini pia amewahi kuifundisha DC Motema Pembe ya nchini humo.

Kupata mengi aliyozungumza kuhusu soka la Tanzania na malengo yake akiwa Yanga, bila kusahau historia na uwezo wake kwa kina, usikose kipindi cha Yanga TV, Ijumaa Aprili 27, 2018) saa 1:00 usiku kupitia Azam Sports 2, ambapo pamoja na mambo mengine, amepania kuwashikisha adabu watani zao wa jadi, Simba SC katika mchezo wa Aprili 29.